top of page
Writer's pictureBranice Nafula

Nguvu Ya Ubunifu, Mitandao Ya Kijamii Na Majukwaa Ya Muziki Kwenye Zinduzi Za Albamu /Ep



Wasanii wamekuwa wakiachia albamu ama EP zao na kufanya wapenzi na mashabiki wa mzuri kupata burudani. Kinachoonekana pia ni kuwa wasanii wamezingatia ubora wa kazi zao, kuanzia utengenezaji hadi jinsi wanavyozitangaza kwa wadau na mashabiki zao kwa lengo la kuweza kufaidika na kazi za mikono yao.

 

Zinduzi za albamu za wasanii kwa miaka ya hivi karibuni zimejawa na ubunifu hadi kufanania zile za nchi za waliondelea, kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakibuni namna mbalimbali za kuwafanya mashabiki zao kuwa tayari kusikiliza na kununua kazi zao pindi zinapotoka.

 

Tuliona jinsi Diamond Platnumz alivyofanya mwaka 2022 alipotoa EP yake ya F.O.A, ambayo alianza kwa kudokeza kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, alitumia vituo vyake vya TV na redio, lakini pia alifanya ‘media tour’ kwenye redio za ndani na nje ya Tanzania kutangaza EP yake, na mafanikio yalionekana kwa jinsi ambavyo iliwafikia watu wengi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

 

Ni wazi kwamba mitandao ya kijamii na majukwaa ya muziki ya kidigitali yamekuwa chachu kubwa sana kwa wasanii kutangaza ujio wa nyimbo zao au hata albamu ama EP zao mpya zinazotoka, wamekuwa wakiwachukua mashabiki zao kwenye safari ya kuelekea zinduzi za albamu ama EP wazokaribia kuzitoa.

 

Hivi karibuni wasanii kama Marioo, Stamina, Maua Sama wameachia kazi zao kwa maana ya albamu na EP, na wametumia njia mbalimbali za ubinifu ili kuhakikisha mashabiki zao wanafikiwa na kazi zao. Maua Sama aliachia EP aliyoipa jina la SAMA, Stamina aliachia albamu aliyoipa jina la Msanii Bora wa Hip Hop na Marioo aliachia albamu pia aliyoipa jina la The God Son.

 

Kila mmoja wao ametumia njia mbalimbali za ubunifu ili kuhakikisha mashabiki zao na wapenzi wa muziki wanawiwa kusikiliza kazi zao. Marioo kabla ya kuzindua albamu yake alidokeza sana kwa kutumia akaunti zake za mitandao ya kijamii, kwa kutambulisha jina la albamu yake, ‘cover’ ya albamu, wasanii aliwowashirikisha, lakini pia aliweza kutumia vyombo vya habari na wadau wa muziki kuhakikisha mashabiki zake wako tayari kuipokea alabamu yake. Siku moja kabla ya kuiachia alifanya shughuli ya kusikiliza albamu yake (listening party) na alitumia pia mitandao ya kijamii kutangaza shughuli hiyo na waalikwa. Na siku alipoiachia alisema kuwa albamu yake Inapatikana kwenye majukwaa yote ya muziki ya kidigitali ikiwemo Mdundo.

 

Stamina nae ambae ameachia albamu yake ya Msanii Bora wa Hip Hop, alitumia mitandao ya kijamii kuwaweka mashabiki na wadau wa muziki tayari kuipokea kazi yake na siku alipoiachia ambayo pia ilikuwa siku yake ya kuzaliwa aliwajuza kuwa albamu yake inapatikana kwenye majukwaa ya muziki ya kidigitali ikiwemo Mdundo. Lakini baada ya kuwa ameshaiachia, ametangaza kufanya ‘album tour’ na atasindikizwa na wasanii baadhi amabao amewashirikisha kwenye albamu yake, na kwa kuanza wataanzia mkoa wa Dodoma.

 

 

Yote haya inonesha umuhimu wa ubunifu, matumizi ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidigitali ya muziki yanavyosaidia wasanii kuhakikisha kazi zao zinzawafikia mashabiki zao na wanafaidika na kazi wanazozitoa. Tunategemea makubwa zaidi kutoka kwa wasanii wetu ikiwemo waliotangaza ujio wa albamu ama EP zao ikiwemo Zuchu, Chino Kidd na wengine.

 

Share maoni yako hapo chini, unaonaje namna wasanii wanatumia ubunifu na majukwaa ya muziki wanapozindua albamu ama EP zao, kuna cha kuongeza?

0 views0 comments

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page